Source : Ippmedia
Posted by: Webmaster on 14-Mar-2010
Bodi ya Wakurugenzi Watendaji wa Benki ya Dunia (WB), imeidhinisha mkopo wenye thamani ya Dola milioni 40 za Marekani kwa ajili ya kufanikisha mradi wa kufadhili ujenzi wa makazi hapa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na WB, fedha hizo zilitolewa kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa (IDA).
Malengo ya mradi huo ni kuanzisha mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, itakayotolewa kwa masharti ya kulipwa katika muda mfupi na mrefu.
Tatizo hilo linaongezeka kila mwaka, ikiwa ni matokeo ya ukosefu wa mikopo ya ujenzi wa makazi, sekta rasmi ya ujenzi wa nyumba za kuishi, kasi ya ukuaji wa idadi ya watu, kuanzishwa na kukua kwa miji.
"Kwa kuimarisha upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya ujenzi wa makazi, fedha hizi zitasaidia kuibua ukuaji bora wa uchumi, ambao matunda yake ni kuwepo ajira na kupunguza umasikini," alisema Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Uganda na Burundi, John Murray McIntire. Kuibuliwa kwa mradi huo kumechochewa na maboresho ya hivi karibuni kuhusu mazingira ya mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba.
Kupitishwa kwa sheria namba 17 ya mwaka 2008 inayohusu nafasi ya mikopo katika kufanikisha ujenzi wa nyumba, imechochea kasi ya serikali kuwa na mfuko wa fedha za ujenzi wa nyumba na kusababisha matarajio makubwa.
Pia, mpango mahususi wa Benki Kuu ya Tanzania (Bot) kwa ajili ya asasi ndogo za fedha, unaziwezesha (asasi) kuwa imara katika sekta ya fedha, kuinufaisha jamii kwa kutumia mgawanyo mdogo wa fedha, hivyo kuwa miongoni mwa mazingira yaliyofanikisha mradi huo.
Kiongozi wa kikosi kazi cha utekelezaji wa mradi wa WB nchini, Michel Noel, alisema soko la mikopo linawatenga watu wengi katika kuboresha makazi yao.
Alisema hali hiyo inaibua haja ya kuwepo mpango bora wa fedha utakaowafikia wasionufaika na mikopo michache inayotolewa sasa, ili wakamilishe ujenzi.
Hii ni mara ya tatu kwa IDA kuidhinisha fedha kwa Tanzania katika kipindi cha mwaka 2009/2010, hivyo kufanya kiasi cha jumla yaka kufikia Dola milioni 250.

